Rapa Diddy Kusomewa Hukumu Oktoba 3 kwa Kesi ya Ukahaba
Rapa na mfanyabiashara maarufu wa Marekani, Sean Combs almaarufu Diddy, amepangiwa rasmi tarehe ya kusomewa hukumu yake kuhusiana na makosa ya biashara ya ukahaba. Jaji Arun Subramanian ametangaza kuwa hukumu hiyo itasomwa Oktoba 3 mwaka huu, ikiwa ni siku ile ile aliyopendekeza wiki iliyopita mara baada ya Diddy kupatikana na hatia kwa makosa mawili makuu yanayohusiana na kusafirisha watu kwa lengo la kujihusisha na ngono. Kulingana na vyanzo vya mahakama, Diddy atasalia kizuizini hadi siku hiyo ya hukumu, hali inayomaanisha kuwa atakuwa amekaa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja kufikia wakati huo. Muda aliokaa rumande unatarajiwa kuzingatiwa katika uamuzi wa mwisho wa kifungo chake. Hii inakuwa hatua nyingine kubwa katika sakata linalomkumba Diddy, ambaye kwa miaka mingi amekuwa mmoja wa majina makubwa katika tasnia ya burudani Marekani. Wadau mbalimbali wa muziki na mashabiki wake wameendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa kesi hii inayotikisa vichwa vya habari kimataifa.
Read More