Cassie Amuomba Hakimu Asimwachilie Diddy kwa Dhamana

Cassie Amuomba Hakimu Asimwachilie Diddy kwa Dhamana

Casandra “Cassie” Ventura, mpenzi wa zamani wa rapa maarufu Sean “Diddy” Combs, amewasilisha ombi rasmi mahakamani akiomba msanii huyo asiachiliwe kwa dhamana, akieleza kuwa usalama wake uko mashakani endapo ataachiliwa kabla ya hukumu kutolewa. Katika barua iliyowasilishwa kwa Jaji Arun Subramanian, Cassie amesema anahofia maisha yake na usalama wa mashahidi wengine waliohusika katika kesi hiyo. Anadai kuwa Diddy ana uwezo mkubwa wa kushawishi, kutisha, au kuzuia ushahidi kutoka kwa mashahidi muhimu ikiwa atakuwa huru nje ya gereza. Kesi dhidi ya Diddy imekuwa gumzo kubwa nchini Marekani, ikihusisha madai mazito ya usafirishaji wa watu kwa ajili ya ngono. Ingawa alisafishwa kwenye mashtaka makubwa ya usafirishaji wa binadamu na uhalifu wa mtandao (racketeering), bado alipatikana na hatia ya makosa mawili madogo yanayohusiana na usafirishaji kwa nia ya kufanya ukahaba. Cassie, ambaye alikuwa mmoja wa mashahidi muhimu, alitoa ushuhuda wa kina mahakamani, akieleza jinsi alivyoathirika wakati wa uhusiano wake na Diddy. Ushuhuda wake uliungwa mkono na mashahidi wengine ambao pia wamewasilisha barua za kuomba Diddy asipewe dhamana hadi kesi hiyo itakapokamilika. Mawakili wa serikali wamesisitiza kuwa Diddy ni mtu mwenye ushawishi mkubwa na mali nyingi, hivyo anaweza kutumia nafasi ya dhamana kuharibu ushahidi au kutoroka. Wamependekeza adhabu ya kifungo cha kati ya miaka minne hadi mitano kwa makosa aliyopatikana nayo. Kwa upande wa utetezi, mawakili wa Diddy wameomba apewe dhamana ya dola milioni moja, huku wakiahidi kuwa atakabidhi pasipoti yake na kuwekwa chini ya uangalizi wa kifaa cha kielektroniki (GPS). Wanasema Diddy hajawahi kukiuka masharti ya mahakama tangu mashitaka yaanze na kwamba ana familia na biashara zinazomfungamanisha na Marekani. Jaji Subramanian bado hajatoa uamuzi kuhusu ombi hilo la dhamana. Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa ndani ya siku chache zijazo, na utakuwa muhimu katika kuamua ikiwa Diddy atasubiri hukumu yake akiwa nje au ataendelea kuzuiliwa gerezani.

Read More
 Suge Knight Amshauri Diddy Kufika Mahakamani na Kusema Ukweli Wake

Suge Knight Amshauri Diddy Kufika Mahakamani na Kusema Ukweli Wake

Rais wa zamani wa Death Row Records, Suge Knight, ambaye amekuwa mpinzani wa muda mrefu wa msanii na mfanyabiashara Sean “Diddy” Combs, amemtaka mwanamuziki huyo maarufu kufika kizimbani na kueleza ukweli wake katika kesi inayomkabili, akiamini kuwa hatua hiyo inaweza kuushawishi vizuri upande wa majaji. Katika mahojiano ya simu na Laura Coates wa CNN, Knight alisisitiza umuhimu wa Combs kujionyesha kama binadamu wa kawaida.  “Ninaamini kama atasimama na kusema ukweli wake, basi atapata nafasi ya kuachiwa,” Knight alisema. “Kama Puffy atasema, ‘Nilikua natumia madawa ya kulevya. Sikuwa na udhibiti wa maisha yangu au nafsi yangu,’ basi ataweza kujihumanisha, na jopo la majaji linaweza kumuelewa.” Knight, ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 28 jela kwa kosa la kuua mtu kwa makusudi kupitia ajali ya gari mwaka 2015, alionya kuwa ukimya unaweza kuathiri kesi ya Combs. “Kama ataendelea kukaa kimya, itaonekana kama anaogopa ukweli. Anatakiwa kuwa na imani na Mungu, avae suruali zake, asimame na aseme ukweli wake,” alisema Knight. Sean “Diddy” Combs amekana mashtaka ya kupanga njama ya uhalifu (racketeering), usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono, na usafirishaji kwa nia ya ukahaba. Ikiwa atapatikana na hatia kwa mashtaka yote, anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Read More
 Mia Asema Diddy Alimdhalilisha Kingono, Atoa Ushahidi Mzito Mahakamani

Mia Asema Diddy Alimdhalilisha Kingono, Atoa Ushahidi Mzito Mahakamani

Aliyekuwa msaidizi wa mwanamuziki na mfanyabiashara maarufu Sean “Diddy” Combs, anayejulikana kwa jina la Mia, amejitokeza mahakamani kutoa ushahidi mzito unaomhusisha mwajiri wake wa zamani na unyanyasaji wa kingono. Mia alieleza mbele ya mahakama jinsi alivyodhalilishwa kingono na Diddy, akisema tukio hilo lilimuacha akiwa na hofu kubwa, aibu na maumivu ya kihisia ambayo bado hayajapona. Alisema kuwa tukio hilo lilikuwa la kutisha na kwamba alihisi hana njia ya kujitetea wala kuondoka katika mazingira hayo. Katika ushahidi wake, Mia alifunguka kuhusu hali ya uoga aliyokuwa nayo wakati huo, akihisi kuwa hangeweza kusema ukweli kwa kuhofia athari za kazi na maisha yake. Alisema aliishi kimya kwa muda mrefu kabla ya kupata ujasiri wa kusimulia yaliyomtokea. Kesi dhidi ya Diddy imeendelea kupata uzito huku mashahidi kadhaa wakijitokeza na madai mbalimbali, yote yakionyesha taswira tofauti ya mtu ambaye kwa muda mrefu ameonekana kama miongoni mwa majina makubwa kwenye muziki na biashara ya burudan Kesi hii imeongeza moto kwenye mjadala unaoendelea kuhusu nguvu, hofu, na unyanyasaji katika sekta ya burudani, hasa ikizingatiwa kuwa Diddy ni mmoja wa majina makubwa kwenye tasnia hiyo. Hata hivyo, Diddy hajatoa tamko rasmi kuhusu madai haya mapya, lakini mawakili wake wamekanusha tuhuma zote zilizowahi kuibuliwa dhidi yake katika kesi nyingine.

Read More