NOCK Yasisitiza Usawa kwa Wanariadha Wote kuelekea Olimpiki
Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki nchini Kenya (NOCK) imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha kila mwanariadha nchini anapewa nafasi sawa ya kushiriki katika mashindano ya kimataifa, ikiwemo Michezo ya Olimpiki ya Vijana ya Dakar na Olimpiki ya Los Angeles mwaka 2028. Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa NOCK, Shadrack Maluki, wakati wa mkutano wake na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Michezo, Dan Wanyama. Maluki alieleza kuwa NOCK inalenga kuhakikisha hakuna talanta inayopuuzwa, huku ikiweka mikakati madhubuti ya kutambua, kukuza na kuendeleza wanamichezo kutoka kila kona ya nchi. Kwa upande wake, Dan Wanyama aliahidi kuwa Bunge litaendelea kushirikiana kwa karibu na NOCK ili kuboresha mazingira ya michezo nchini. Alisisitiza umuhimu wa kuwa na sera imara, miundombinu bora, pamoja na uwekezaji wa kutosha katika maendeleo ya michezo, ili kuhakikisha Kenya inaendelea kung’ara katika majukwaa ya kimataifa. Mkutano huo ni sehemu ya juhudi za pamoja kati ya wadau wa michezo na serikali kuhakikisha kuwa Kenya inatuma timu zenye ushindani mkubwa kwenye mashindano yajayo ya kimataifa, huku vijana wakipewa nafasi ya kujifunza, kushindana, na kuiwakilisha nchi kwa fahari.
Read More