Tems Aweka Historia kwa Kutumbuiza Katika Fainali ya FIFA Club World Cup
Mwanamuziki nyota kutoka Nigeria, Tems, ameandika historia mpya usiku wa kuamkia leo kwa kuwa msanii wa kwanza wa Kiafrika kutumbuiza kwenye fainali ya Kombe la Dunia la Vilabu (FIFA Club World Cup), hatua inayotajwa kuonyesha wazi ukubwa wa kipaji chake na kuendeleza hadhi ya muziki wa Afrika kwenye jukwaa la kimataifa. Tems alitumbuiza katika burudani ya mapumziko (Halftime Show) sambamba na mastaa wa kimataifa, Doja Cat kutoka Marekani na J Balvin wa Colombia katika tukio lililofanyika kwenye Uwanja wa MetLife, New Jersey, Marekani. Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa michuano hiyo ya Club World Cup kuandaa onyesho la burudani katikati ya mchezo (halftime show), hivyo kufanya tukio hilo kuwa la kihistoria katika dunia ya soka na burudani. Burudani hiyo ya kuvutia ilifanyika wakati wa fainali ya michuano hiyo, ambapo klabu ya Chelsea FC kutoka England iliibuka mshindi dhidi ya mabingwa wa Ufaransa, Paris Saint-Germain (PSG), na kutwaa taji la Kombe la Dunia kwa ngazi ya vilabu. Uwepo wa Tems katika jukwaa hilo umepongezwa na mashabiki na wadau wa sanaa kama hatua kubwa kwa wasanii wa Afrika, huku wengi wakisema kwamba anazidi kuvunja mipaka na kupeperusha bendera ya bara la Afrika kwa mafanikio makubwa. Tems, anayefahamika kwa sauti yake ya kipekee na uandishi wa nyimbo wa hali ya juu, amekuwa akivuma kimataifa kwa miaka ya hivi karibuni, na sasa amejiweka kwenye ramani ya wasanii wa dunia wanaotumbuiza kwenye matukio makubwa ya kihistoria.
Read More