Terence Creative Ateuliwa Katibu Mkuu wa Chama cha Watayarishi wa Maudhui Mtandaoni Kenya (DCCAK)

Terence Creative Ateuliwa Katibu Mkuu wa Chama cha Watayarishi wa Maudhui Mtandaoni Kenya (DCCAK)

Mchekeshaji maarufu na mtayarishaji wa maudhui mtandaoni, Terence Creative, ametangazwa rasmi kuwa Katibu Mkuu (Secretary General) wa Digital Content Creators Association of Kenya (DCCAK) – chama kipya kinacholenga kutetea maslahi ya watayarishi wa maudhui nchini. Uteuzi huo ulifanyika katika hafla rasmi iliyowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kidijitali, ambapo pia walitambulishwa wajumbe wengine wa chama hicho, akiwemo Nasra Yusuff, Director Trevor, Sammy Kioko, na Claudia Naisabwa ambao watafanya kazi kwa karibu na Terence katika kuongoza harakati za chama hicho. DCCAK inalenga kuleta mabadiliko katika tasnia ya utayarishaji maudhui mtandaoni kwa kuweka sera bora, kushirikiana na serikali na sekta binafsi, pamoja na kutoa mafunzo, mikakati ya ukuaji, na ulinzi wa kazi za watayarishi. Akizungumza baada ya uteuzi wake, Terence alisema:  “Hii ni hatua kubwa siyo tu kwa mimi binafsi bali kwa jamii nzima ya watayarishi wa maudhui. Tunahitaji sauti ya pamoja ili kuhakikisha tunatambulika, tunalindwa, na tunapata mazingira bora ya kazi.” Watayarishi wa maudhui wameibuka kuwa sehemu muhimu ya uchumi wa kidijitali nchini Kenya, lakini wengi wao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za kisheria, kifedha na kimaudhui kutokana na kukosekana kwa mwongozo rasmi au uwakilishi thabiti. Kupitia uongozi wa Terence na timu yake, DCCAK inatarajiwa kuwa jukwaa la mabadiliko chanya katika uandaaji wa maudhui, kuendeleza vipaji vipya, na kuhimiza ubunifu unaozingatia maadili na haki za kiutendaji.

Read More