META Yapiga Marufuku Wizi wa Maudhui Mitandaoni

META Yapiga Marufuku Wizi wa Maudhui Mitandaoni

Kampuni ya Meta, inayomiliki mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram, na Threads, imetangaza kuwa inaanza kuchukua hatua kali dhidi ya akaunti ambazo zinashiriki au kuchapisha upya (repost) maudhui ya akaunti nyingine bila ruhusa au kibali. Kupitia taarifa rasmi, Meta imesema kuwa sera hii inalenga kulinda haki miliki za watumiaji, kuhamasisha ubunifu wa asili, na kupunguza wizi wa maudhui mtandaoni. Akaunti zitakazobainika kukiuka sera hii zitawekewa vikwazo vya kufikia watumiaji wengine (reach restriction), kusimamishwa kwa muda, au hata kufungiwa kabisa. “Hii ni hatua ya kuhakikisha kuwa watu wanaotumia muda na juhudi zao kuunda maudhui wanapewa heshima na ulinzi wanaostahili,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo. Watumiaji sasa wanahimizwa kuhakikisha wanapata kibali kabla ya kushiriki tena maudhui ya wengine, hasa ya akaunti za kibiashara, wasanii, au waandishi wa habari. Hatua hii imepokelewa kwa hisia mseto, huku baadhi ya watumiaji wakiiunga mkono kwa kusema inalinda ubunifu, ilhali wengine wakieleza wasiwasi kuwa huenda ikapunguza usambazaji wa taarifa muhimu na burudani mtandaoni. Meta inatarajiwa kuanza kutekeleza hatua hizi kikamilifu katika siku chache zijazo, huku ikiwataka watumiaji kusoma na kuelewa masharti ya matumizi ya mitandao yao kwa kina.

Read More