Eddy Kenzo Kutatua Mgogoro wa Ofisi za UMA Zilizofungwa kwa Madeni
Rais wa Shirikisho la Wanamuziki Uganda (UNMF) na mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Uganda katika masuala ya ubunifu, Eddy Kenzo, ameahidi kuingilia kati na kusaidia Chama cha Wanamuziki Uganda (UMA) kurejeshewa ofisi zake zilizofungwa kutokana na deni la kodi. Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini humo, Kenzo amesema hatua hiyo inalenga kutunza heshima ya taasisi ya UMA ambayo, kwa mujibu wake, imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya muziki nchini Uganda kabla ya kuanzishwa kwa UNMF. “Hatuwezi kuwaacha katika hali hii. UMA walifanya kazi kubwa kabla sisi hatujaja. Tutaingilia kati na kuona namna ya kuhakikisha ofisi zao zinafunguliwa tena,” alisema Kenzo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha ndani. Kauli yake imekuja kufuatia hatua ya Kituo cha Kitaifa cha Utamaduni cha Uganda (UNCC), kinachomiliki jengo la National Theatre, kufunga rasmi ofisi za UMA kwa kile kilichoelezwa kuwa malimbikizo ya kodi ya karibu mwaka mmoja. Hatua hiyo imeathiri moja kwa moja uendeshaji wa shughuli za chama, huku ofisi za viongozi wakuu kama Cindy Sanyu (Rais wa UMA) na Phina Masanyalaze (Katibu Mkuu) zikiwa zimefungwa na kuwekewa zuio la kuingia. UMA, chini ya Cindy, imekuwa ikikosoa waziwazi uongozi wa UNMF na haswa Kenzo, huku mvutano kati yao ukijidhihirisha mara kadhaa katika majukwaa ya umma. Hata hivyo, Kenzo amechukua hatua ya kukutana na viongozi husika ili kushughulikia suala hilo kwa njia ya amani, akisema huu si wakati wa kutazama tofauti bali kushikamana kwa maslahi ya wanamuziki wote nchini Uganda. Sakata hili linaendelea kuwavutia wadau wengi wa sekta ya burudani nchini Uganda, huku wengi wakisubiri kuona ikiwa hatua ya Kenzo itazaa matunda na kumaliza mgogoro unaoathiri ustawi wa chama kongwe cha wanamuziki nchini.
Read More