Goddy Tennor Adai Kuwa Miongoni mwa Waanzilishi wa Miondoko ya Arbantone
Msanii na mtayarishaji wa muziki Goddy Tennor amedai kuwa yeye pamoja na wasanii wenzake Tipsy Gee, Soundcraft na Kappy ndio waanzilishi wa miondoko ya muziki wa Arbantone, mtindo unaozidi kushika kasi miongoni mwa vijana nchini Kenya. Akizungumza katika mahojiano maalum, Tennor alisema kuwa wazo la kuanzisha Arbantone lilizaliwa katika mazingira ya mtaa, likichochewa na haja ya kuwasilisha sauti ya vijana wa Nairobi kwa kutumia mitindo mipya ya midundo na lugha ya kizazi kipya. “Mimi, Tipsy Gee, Soundcraft na Kappy tulianzisha Arbantone. Tulikuwa tukikutana studio mara kwa mara tukijaribu vitu vipya hadi tukapata sound ya kipekee,” alieleza. Tennor aliongeza kuwa mtindo huo ulitokana na mchanganyiko wa muziki wa gengetone, trap, na midundo ya mtaa, na kwamba walilenga kuunda aina ya muziki unaoeleweka kitaifa lakini unaoweza kufika ngazi za kimataifa. Kwa mujibu wa Tennor, dhamira yao haikuwa kutafuta sifa, bali kuunda jukwaa la muziki ambalo lingebeba utambulisho wa vijana wa Nairobi. Alieleza kuwa mchanganyiko wa sauti ya mtaa na midundo ya kisasa ndio uliwapa msukumo wa kuunda aina hiyo ya muziki ambayo baadaye ilijulikana kama Arbantone. Hata hivyo, si kila mtu anakubaliana na kauli ya Tennor. Mwaka 2023, mtayarishaji maarufu Motif Di Don alidai kuwa ndiye mwanzilishi wa mtindo wa muziki unaofanana kwa jina tofauti la Urbantone. Ingawa Motif hakufafanua zaidi kuhusu mchango wa wasanii wengine, taarifa yake inaendelea kuibua mijadala kuhusu nani hasa alianza mtindo huo. Licha ya mvutano huo, Arbantone kwa sasa ni mojawapo ya mitindo ya muziki inayokua kwa kasi zaidi nchini. Mtindo huu umechangia kuibuka kwa wasanii kadhaa chipukizi ambao wanatawala majukwaa ya mitandao ya kijamii na redio. Miongoni mwao ni Maandy, YBW Smith, Soundkraft, Sean MMG, Lil Maina, Ebola Mkuu, Goddy Tennor mwenyewe, Kappy na Tipsy Gee. Muziki wa Arbantone umejipatia sifa kwa kuwasilisha maudhui ya maisha ya kila siku ya vijanakutoka kwenye uhusiano wa kimapenzi hadi changamoto za kijamii kwa lugha ya mtaa inayovutia hadhira kubwa. Wachambuzi wa muziki wanasema kuwa mvutano kuhusu nani aliyeanzisha Arbantone ni wa kawaida katika hatua za awali za maendeleo ya mtindo wowote mpya. Hata hivyo, wanakubaliana kuwa miondoko hiyo imefungua ukurasa mpya katika muziki wa Kenya na huenda ikawa sehemu ya utambulisho wa muziki wa kisasa Afrika Mashariki kwa miaka mingi ijayo.
Read More