“Sihitaji Pesa, Nahitaji Fursa” – Msanii Visita Aomba Msaada wa Vifaa
Msanii maarufu Visita, ambaye amewahi kung’ara kwenye tasnia ya muziki nchini Kenya, ameacha wengi wakiwa na huzuni na mshangao baada ya kufichua changamoto kali za maisha alizopitia, ambazo zilimsukuma hadi katika hali ya msongo wa mawazo na kuishi maisha ya uraiani kwa muda. Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na Obinna TV, Visita alisema maisha yalibadilika ghafla na kuanza kumlemea, hali iliyomfanya ajikute akilala nje, akiwa na njaa na kufungiwa nyumba kwa miezi mitatu. “Nilifikia hatua mbaya sana kimaisha. Nilikua na njaa, nimefungiwa nyumba kwa miezi mitatu, sina pa kwenda. Nilihisi nimevunjika kabisa, lakini ndani yangu nilijua siwezi kubaki hapo nilikua napambana na nafsi yangu kila siku,” Visita alieleza kwa uchungu. Akiwa na uso wa matumaini lakini uliobeba maumivu ya ndani, Visita alisema alipitia hali ya kukosa chakula kwa siku kadhaa hadi majirani walipoanza kumsaidia chakula na mahitaji ya msingi. Hali hiyo iliendelea hadi msamaria mwema mmoja alipojitokeza na kumpatia chumba kidogo cha kujishikilia, si biashara, bali sehemu ya kujisitiri kwa muda huku akijaribu kujijenga upya. “Yule msamaria aliniona nimeishiwa, akanipa chumba kidogo cha kutumia kama makazi. Ndicho ninachoishi sasa, na ndicho kimenisaidia nisiangamie kabisa,” alisema kwa sauti ya shukrani. Visita, ambaye hapo awali alikuwa mmoja wa wasanii waliotoa burudani kwa nguvu katika majukwaa ya muziki, anasema ikiwa angepata vifaa vya muziki kama spika, laptop au mixer hata vya bei nafuu au vilivyotumika (second-hand), anaweza kuanza kufanya kazi ya muziki tena na kujipatia kipato cha kulipa kodi, kula, na hata kujiendeleza. “Naamini nikisaidiwa hata na vifaa vya second-hand, naweza kujimudu, kujilipa kodi na kupata chakula. Sitaki kurudi tena kule nilikotoka,” aliongeza kwa matumaini. Kwa sasa, Visita anaendelea kuishi kwa neema ya watu wachache wanaomuunga mkono, huku akitoa wito kwa wasamaria wema na mashirika ya sanaa kumsaidia arudi kwenye miguu yake. Ameeleza kuwa bado ana kipaji na ndoto za kubadilisha maisha yake na hata kuwatia moyo vijana wengine wanaokumbana na changamoto kama zake. Iwapo ungependa kumsaidia Visita, unaweza kuwasiliana naye kupitia maelezo ya mawasiliano aliyoyatoa kwa Obinna TV au kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Read More