Wema Sepetu Aitwa na Bodi ya Filamu Nchini Tanzania Kisa Mavazi
Bodi ya Filamu Tanzania imemwita rasmi msanii maarufu wa filamu za Bongo, Wema Sepetu, kufika katika ofisi zao kwa ajili ya mahojiano kufuatia kusambaa kwa picha jongevu (video clips) mitandaoni ambazo zinadaiwa kukiuka maadili ya kazi za sanaa nchini. Katika taarifa iliyotolewa na bodi hiyo, imeelezwa kuwa video hizo zinamuonesha Wema akiwa amevaa mavazi yasiyo na staha, jambo ambalo limeibua mjadala mkubwa mitandaoni na kuibua wasiwasi miongoni mwa wadau wa tasnia ya filamu na jamii kwa ujumla. Bodi hiyo imekumbusha wasanii wote Nchini Tanzania kuzingatia maadili, sheria na kanuni za uendeshaji wa kazi za sanaa, hasa katika enzi hizi ambapo maudhui huenea kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii. Wema Sepetu, ambaye ni mmoja wa waigizaji maarufu na wenye ushawishi mkubwa nchini humo, bado hajatoa kauli rasmi kuhusiana na wito huo wa Bodi. Hata hivyo, mashabiki wake wamekuwa wakitoa maoni tofauti, baadhi wakimtetea na wengine wakihitaji afuate misingi ya maadili ya kazi za sanaa.
Read More