Eric Omondi Atoa Kauli Kuhusu Agizo la Rais Ruto la Risasi Mguuni

Eric Omondi Atoa Kauli Kuhusu Agizo la Rais Ruto la Risasi Mguuni

Mchekeshaji maarufu Eric Omondi ameibua hisia mseto mitandaoni baada ya kutoa kauli fupi lakini nzito kufuatia agizo la Rais William Ruto, linalowataka maafisa wa usalama kuwafyatulia risasi mguuni wale wanaohusika na uharibifu wa mali ya umma. Akiwa kwenye Ibada ya mazishi ya marehemu Boniface Mwangi Kariuki, Eric alionesha kusikitishwa na mwelekeo wa kisiasa na kijamii nchini, akisema kuwa taifa linahitaji maombi zaidi ya chochote kingine kwa sasa. Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya Rais kutoa agizo hilo akiwa katika hafla ya hadhara. Agizo la Rais limezua mjadala mkubwa nchini, huku baadhi ya wananchi na wanaharakati wa haki za binadamu wakieleza wasiwasi wao kuhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi na uwezekano wa kukiukwa kwa haki za raia. Eric Omondi, ambaye amejitokeza mara kadhaa kuikosoa serikali na kuongoza harakati za kijamii, anaonekana kuashiria hali ya taharuki na sintofahamu inayozidi kushika kasi nchini. Wafuasi wake wengi wamelitafsiri tangazo lake kama kilio cha kutafuta amani na busara katika uongozi wa taifa. Mjadala kuhusu agizo la Rais unaendelea kushika kasi, huku wadau mbalimbali wakitoa maoni yao kuhusu uhalali, athari na mwelekeo wa hatua hiyo kwa mustakabali wa haki za binadamu na demokrasia nchini.

Read More
 Akothee Amwandikia Rais Ruto: “Tufungue Mlango wa Mazungumzo”

Akothee Amwandikia Rais Ruto: “Tufungue Mlango wa Mazungumzo”

Mwanamuziki, mfanyabiashara, na mwanaharakati wa kijamii Akothee maarufu kama Rais wa Akina Mama Wasio na Wenzi, ameandika barua ya wazi kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, akitoa kilio cha kina kwa niaba ya akina mama, vijana, wazazi, na wajasiriamali nchini. Katika barua hiyo yenye hisia nzito, Esther anasema haandiki kama mtu maarufu tu, bali kama mzazi anayeishi na vijana wa kizazi cha Gen Z, ambao wamekuwa mstari wa mbele katika maandamano ya hivi karibuni kote nchini. “Nakuandikia si tu kama raia, bali kama mama, mama asiye na mwenzi wa vijana wa Gen Z – na kama Mkenya ambaye bado anaamini katika roho ya taifa hili,” alianza kwa maneno yenye kugusa moyo. Esther anaelezea hali ya taifa kwa sasa kuwa ya kusikitisha, mitaa imejaa hofu, anga limefungwa na huzuni, na familia pamoja na biashara ziko katika hali ya taharuki. Anasema vijana na wananchi kwa ujumla hawatafuti tu mabadiliko ya sera, bali wanalilia usalama, uthabiti, na uongozi unaosikiliza. “Wakenya sasa hawapigi kelele kwa mabadiliko tu. Wanapaza sauti kwa ajili ya usalama, uthabiti na uelewa. Wanataka uongozi unaosikiliza; nchi ambayo watoto wao wanaweza kwenda shule bila vurugu, biashara kufunguliwa bila hofu ya uporaji, na familia zisizopoteza wapendwa kwa risasi au kipigo,” alieleza kwa uchungu. Esther pia anahoji uhalali wa taifa kuhubiri amani ulimwenguni huku picha halisi ya ndani ikionyesha vurugu, mauzoo ya matumaini, na uharibifu wa kiuchumi unaowatesa wananchi wa kawaida. Akitilia mkazo kuwa barua hiyo si ya lawama, bali ya uwajibikaji wa pamoja, anamtaka Rais kuchukua hatua ya kidiplomasia ya kuanzisha mazungumzo ya kweli. “Hili si suala la lawama. Ni kuhusu uwajibikaji wa pamoja. Tukivutana, tunapoteza sote. Na anayepoteza zaidi ni Kenya.” Kama mama, anasema anaelewa kiu ya vijana kusikilizwa, ndiyo maana baadhi yao walijaribu kuingia bungeni. Sio kwa fujo, bali kama njia ya kuonyesha kutotambuliwa kwao katika maamuzi ya taifa. Alihitimisha barua hiyo kwa ombi la moja kwa moja kwa Rais, kuwakutanisha na wazazi, akina mama, na vijana Ikulu kwa mazungumzo ya wazi. “Nakuomba kwa unyenyekevu unikubalie nafasi ya kusikilizwa, si kwa ajili yangu tu, bali kwa ajili ya mama wote, wazazi, na vijana wetu. Tufungulie mlango. Tuweke tofauti kando. Tufikirie pamoja. Natumaini mazungumzo yanaweza kuokoa roho ya taifa hili.” Barua hiyo imeendelea kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, ambapo wengi wameisifu kama sauti ya ujasiri, huruma, na matumaini, sauti inayozungumza kutoka moyoni mwa mzazi wa kawaida hadi juu ya meza ya mamlaka.

Read More
 Wilbroda Atoa Wito kwa Rais Ruto Asikie Kilio cha Wananchi

Wilbroda Atoa Wito kwa Rais Ruto Asikie Kilio cha Wananchi

Mwigizaji maarufu wa Kenya, Wilbroda, ameibua hisia kali mtandaoni baada ya kueleza kwa uchungu hali ngumu ambayo wananchi wanapitia chini ya utawala wa sasa, huku akimpelekea Rais William Ruto ujumbe wa moja kwa moja akimtaka asikilize kilio cha wananchi. Kupitia video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Wilbroda alieleza kuwa bado kuna muda wa miaka miwili na nusu kabla ya uchaguzi mwingine, na angetamani sana kuona Rais akisikia sauti ya wananchi na kurekebisha baadhi ya mambo ambayo, kwa mtazamo wake, yameathiri maisha ya wananchi wa kawaida. “Ningependa sana askize ground, this guy still has two and a half years, I wish he would listen to the people and reverse a lot of things that have happened in this country. People are going through so much,” alisema Wilbroda kwa hisia kali. Kauli yake imeibua maoni tofauti kutoka kwa Wakenya mtandaoni, wengi wakimuunga mkono na wengine wakimtaka azingatie usawa katika uchambuzi wake. Lakini ujumbe wake umeeleweka wazi: maisha yamekuwa magumu kwa mwananchi wa kawaida, na kuna haja ya serikali kuchukua hatua kurekebisha hali hiyo. Wilbroda, anayefahamika kwa ucheshi na uigizaji wa kuvutia, amekuwa sauti ya watu wengi mitandaoni, na kwa mara hii, ameamua kutumia umaarufu wake kuangazia masuala ya kijamii yanayoathiri mamilioni ya Wakenya.

Read More