William Saliba Kukaa Arsenal Mpaka 2030 Baada ya Kukubali Mkataba Mpya
Beki wa klabu ya Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, William Saliba, ameripotiwa kukubali kusaini mkataba mpya wa miaka mitano na miamba hiyo ya Ligi Kuu ya England (EPL), hatua itakayomuweka Emirates hadi mwaka 2030. Saliba, ambaye amekuwa nguzo muhimu katika safu ya ulinzi ya Arsenal, alikuwa amesalia na miaka miwili kwenye mkataba wake wa sasa unaotarajiwa kumalizika mwezi Juni 2027. Hata hivyo, uongozi wa Arsenal umeamua kumfunga kwa muda mrefu zaidi, kufuatia kiwango chake bora ambacho kimevutia vilabu vikubwa barani Ulaya, ikiwemo Real Madrid ya Uhispania. Kwa mujibu wa duru za ndani ya klabu hiyo ya Kaskazini mwa London, mkataba huo mpya unatarajiwa kutangazwa rasmi katika siku chache zijazo, huku mashabiki wakitarajia kuendelea kumuona beki huyo mwenye kasi na akili ya mchezo akiwa sehemu ya kikosi cha kwanza kwa miaka mingi ijayo. Tangu kurejea kutoka kwa mkopo msimu wa 2022/23, Saliba amekuwa mchezaji wa kuaminiwa na kocha Mikel Arteta, akicheza nafasi ya beki wa kati kwa utulivu mkubwa, na kushirikiana kwa mafanikio na Gabriel Magalhães katika safu ya ulinzi.
Read More