Familia ya Zee Cute Yatoa Taarifa Rasmi Kuhusu Afya Yake
Familia na uongozi wa msanii maarufu wa muziki, Zee Cute, wametoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari, mashabiki, na wadau wa tasnia ya muziki, wakifafanua kuwa msanii huyo kwa sasa yuko chini ya uangalizi maalum na matibabu kutokana na changamoto za kiafya, hasa zinazohusiana na afya ya akili. Katika taarifa hiyo iliyotolewa na meneja wake, Baraka Frank, imesema kuwa familia na timu ya usimamizi wanajitahidi kuhakikisha Zee Cute anapata huduma bora za afya na mapumziko ya kutosha ili aweze kupona na kurejea katika hali yake ya kawaida, akiwa na nguvu mpya za kuendelea na kazi zake za muziki. “Tunatoa taarifa hii kwa uwazi ili kuendeleza juhudi za kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kulinda na kuenzi afya ya akili, hasa kwa vijana na wasanii ambao mara nyingi hukumbana na mazingira yenye shinikizo kubwa,” imesema taarifa hiyo. Familia na meneja pia wamewataka watu wote kutoa msaada, faraja, na mazingira salama kwa wale wanaopitia changamoto za afya ya akili, huku wakitoa shukrani za dhati kwa mashabiki, wasanii wenzake, na wadau wote waliotoa salamu za pole, sala, na maneno ya faraja katika kipindi hiki kigumu. Taarifa hiyo imesema kuwa taarifa zaidi kuhusu maendeleo ya afya ya Zee Cute zitatolewa kupitia kurasa zake halali za mitandao ya kijamii, huku wakisisitiza radhi kwa usumbufu wowote unaoweza kujitokeza katika shughuli za muziki wakati huu. Meneja Baraka Frank hata hivyo amewashukuru mashabiki kwa upendo na maombi yao, na kusema kuwa kwa mshikamano na matumaini, wanaamini msanii atavuka kipindi hiki kigumu.
Read More