
Msanii maarufu wa muziki wa pop, Taylor Swift, na nyota wa NFL kutoka timu ya Kansas City Chiefs, Travis Kelce, wametangaza rasmi uchumba wao juzi Agosti 26, 2025.
Kupitia kurasa zao za Instagram, wawili hao wamechapisha picha wakionekana katika dimbwi zito la mapenzi. Katika maelezo ya picha hizo, waliandika kwa ucheshi, “Mwalimu wako wa Kiingereza na mwalimu wako wa mazoezi ya viungo wanafunga ndoa.” Kauli hiyo ya kifurushi cha maneno imeonyesha upekee wa uhusiano wao na kuleta msisimko zaidi kwa mashabiki wanaowafuatilia.
Uhusiano wao ulianza mwaka 2023, baada ya Kelce kufichua kwenye podcast kuwa alijaribu kumpa Swift bangili yenye namba yake ya simu wakati wa tamasha lake la Eras Tour, ingawa hakufanikiwa. Baada ya hapo, wawili hao walianza kuonekana mara kwa mara pamoja kwenye michezo ya Kansas City Chiefs, ikiwemo Super Bowl, na hata walishiriki pamoja katika kipindi maarufu cha “Saturday Night Live.”
Taylor Swift pia alionyesha dalili za uhusiano wao kupitia albamu yake ya mwaka 2024, The Tortured Poets Department, hasa katika nyimbo kama “The Alchemy” na “So High School” ambazo zilionekana kumrejelea mpenzi wake. Hata hivyo, tarehe rasmi ya harusi bado haijatangazwa, lakini mashabiki wao wamefurika kwenye mitandao ya kijamii kuwatumia pongezi na kuonyesha furaha kwa hatua hii mpya katika maisha ya wawili hao maarufu