
Mtandao wa kijamii wa Threads, unaomilikiwa na kampuni ya Meta, umetangaza rasmi uzinduzi wa kipengele kipya kinachowaruhusu watumiaji wake kuandika maandishi marefu zaidi hadi herufi 10,000 katika chapisho moja.
Hatua hii inakuja kama sehemu ya juhudi za Threads kujiimarisha kama jukwaa la maudhui ya kina na mijadala ya kimaudhui, tofauti na mitandao mingine inayoweka mipaka ya urefu wa maandishi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Meta, kipengele hiki kipya kitawawezesha watumiaji, wakiwemo wanahabari, wanablogu, waandishi wa habari za kisiasa, na wanaharakati wa kijamii, kuchapisha maudhui ya kina bila kulazimika kuyagawanya katika post nyingi au kutegemea viungo vya nje.
Hatua hii pia inaashiria ushindani wa moja kwa moja na majukwaa kama X (zamani Twitter), ambalo liliongeza ukomo wa herufi kwa baadhi ya watumiaji wake wa kulipia, pamoja na Substack Notes na LinkedIn, ambayo inawaruhusu watumiaji kuandika maudhui ya kitaaluma.
Uzinduzi huu unafanyika wakati Threads ikiendelea kushika kasi kama jukwaa jipya linalowavutia mamilioni ya watumiaji waliokuwa wakitafuta mbadala wa Twitter, kufuatia mabadiliko ya sera na mmiliki wake Elon Musk.
Kwa sasa, kipengele hiki kinapatikana kwa watumiaji wote wa Threads waliopo katika toleo jipya la programu hiyo, kwenye Android na iOS, huku wakihimizwa kuendelea kutoa mrejesho kuhusu matumizi yake.