
Timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande Shujaa, imefuzu kwa mechi ya fainali katika mashindano ya raga ya Singapore baada ya kuitandika Uhispania kwa alama 12-5 kwenye mechi ya nusu fainali ya kwanza. Timu hiyo inayofunzwa na Kevin Wambua, sasaitachuana na Fiji kwenye mechi ya fainali leo alasiri.
Shujaa ilianza mechi hiyo ya nusu fainali kwa kishindo huku mchezaji Patrick Odongo akifungia alama tano katika dakika ya mwanzo. Nygel Amaitsa akaongeza alama mbili na kuiweka Kenya kifua mbele kwa alama 7-0 katika dakika mbili za mwanzo. Odongo kisha akafunga alama tano zaidi katika dakika ya 8 na hivyo kuongeza uongozi wa Kenya kuwa 12-0 kufikia kipindi cha mapumziko.
Uhispania kisha ikajibu katika dakika ya 13 kwa kufunga alama tano na hivyo mechi hiyo ikakamilika kwa alama 12-5. Fiji ilifuzu kwa mechi ya fainali baada kuishnda Argentina kwa alama 33-24 na kushinda mechi ya nusu fainali ya pili.