
Mtandao wa burudani wa TMZ umechapisha picha ya mfungwa anayeitwa Santino Casio, anayeshukiwa kumshambulia kwa kisu rapa Tory Lanez akiwa gerezani. Kwa mujibu wa TMZ, Casio anatumikia kifungo cha maisha gerezani kwa kosa la mauaji na anatajwa kuwa na historia ya matukio ya vurugu tangu alipoanza kutumikia kifungo chake.
Tukio hilo la kushangaza liliripotiwa kutokea siku ya Jumatatu saa 1:20 asubuhi (7:20 a.m) katika gereza la North Kern, California, ambapo Tory Lanez alishambuliwa na kuchomwa kisu mara 14 kwenye maeneo mbalimbali ya mwili wake ikiwemo kichwani, kifuani, na mgongoni.
Chanzo cha karibu na tukio hilo kimeripoti kuwa Tory aliwekwa kwenye mashine ya kupumua mara baada ya tukio kutokana na majeraha makubwa, lakini taarifa za hivi karibuni zinaeleza kuwa anaendelea vizuri akiwa katika Hospitali ya North Kern Medical Center.
Tukio hili limeibua maswali kuhusu usalama wa wafungwa maarufu ndani ya magereza ya Marekani, hasa ikizingatiwa kuwa Santino Casio anatajwa kuwa tayari amehusika katika matukio mengine ya fujo akiwa jela.
Tory Lanez, ambaye anatumika kifungo cha miaka 10 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumpiga risasi mwanamuziki Megan Thee Stallion mnamo Julai 2020, huenda sasa akahamishwa kutoka gereza hilo kwa ajili ya usalama wake. Ripoti zinaonyesha kuwa endapo atarejeshwa tena North Kern, ulinzi wake utaimarishwa kwa kiwango cha juu zaidi.
Hadi sasa, mamlaka ya magereza bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu sababu ya shambulio hilo au hatua zitakazochukuliwa dhidi ya Santino Casio.