
Msanii mashuhuri wa Mugithi na afisa wa polisi, Samuel Muchoki almaarufu Samidoh, ameibua gumzo mitandaoni baada ya kuchapisha ujumbe tata kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, muda mfupi baada ya kuhamishwa kazini.
Kupitia Instagram, Samidoh aliandika: “When injustice becomes law, resistance becomes duty!”, kauli yenye uzito inayohusishwa na upinzani dhidi ya udhalimu.
Ujumbe huo umetafsiriwa na wengi kama ishara ya kutoridhishwa na hatua ya uhamisho wake kutoka Makao Makuu ya Polisi wa Mkoa wa Kati hadi Kitengo Maalum cha Kukabiliana na Wizi wa Mifugo (ASTU) kilichopo Gilgil, Kaunti ya Nakuru.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, uhamisho wa Samidoh unahusishwa na tukio la Mei 16 ambapo alionekana akitumbuiza huku umati ukipiga kelele za kisiasa ya “Wantam”, kauli inayodaiwa kupinga utawala wa Rais Ruto. Tukio hilo lilisambaa sana mitandaoni.
Ingawa Inspekta Jenerali Douglas Kanja alieleza kuwa uhamisho huo ni wa kawaida, taarifa za ndani zinaeleza kuwa ni hatua ya kinidhamu kwa kukiuka kanuni zinazokataza polisi kushiriki katika siasa.
Mashabiki wa Samidoh wamegawanyika baadhi wakimtia moyo kuendelea na kazi ya polisi kwa nidhamu, huku wengine wakimtaka aachane na kazi hiyo na kujikita kikamilifu katika muziki, ambapo tayari ameonyesha mafanikio makubwa.
Kwa sasa, Samidoh anasubiri matokeo ya uchunguzi wa kinidhamu, hatua inayoweza kuathiri mustakabali wake katika Jeshi la Polisi. Ujumbe wake wa mafumbo unaendelea kuibua mjadala mpana, huku wengi wakisubiri kwa hamu kuona hatua atakayochukua kama msanii, raia, au afisa wa sheria.