Gossip

Vera Sidika Ajibu Ukosoaji Kuhusu Kumruhusu Brown Mauzo Kuwaona Watoto Wao

Vera Sidika Ajibu Ukosoaji Kuhusu Kumruhusu Brown Mauzo Kuwaona Watoto Wao

Mrembo maarufu kutoka Kenya, Vera Sidika, ameweka wazi msimamo wake baada ya kukosolewa kwa uamuzi wake wa kumruhusu aliyekuwa mpenzi wake, mwanamuziki Brown Mauzo, kutumia muda na watoto wao nyumbani kwake.

Kupitia Inst story yake, Vera amesema hajawahi kumtegemea Mauzo kwa msaada wa kifedha na kwamba jambo analolipa kipaumbele ni uwepo wake kama baba katika maisha ya watoto wao. Amebainisha kuwa yeye mwenyewe alikulia kwenye familia yenye wazazi wote wawili, jambo lililomfanya atamani watoto wake wapate malezi yenye upendo na uwepo wa baba, bila kujali changamoto za kifedha.

Akizungumzia dhamira ya Mauzo kama mzazi, Vera amesema amewahi kushuhudia jinsi alivyovunjika moyo baada ya kuzuiwa kumuona mtoto wake na mama wa mtoto wake kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita. Kwa mujibu wake, hali hiyo ilionyesha wazi jinsi anavyothamini nafasi yake kama baba na hamu yake ya kuwa karibu na watoto wake.

Aidha, Vera amekosoa vikali tabia ya baadhi ya akina mama kuwazuia baba kuona watoto wao kwa sababu ya changamoto za kifedha. Alisema kufanya hivyo ni kitendo cha ubinafsi kwa kuwa kinawanyima watoto nafasi ya kupokea upendo na malezi ya baba zao.

Kauli ya Vera imezua mjadala mitandaoni, baadhi ya watu wakimsifu kwa ukomavu na mtazamo wake chanya kuhusu malezi ya pamoja, huku wengine wakisisitiza kuwa majukumu ya kifedha nayo ni sehemu muhimu ya malezi ya mzazi.