
Mwanamuziki wa Kenya anayeishi Marekani, Victoria Kimani, amefichua tukio la kusikitisha ya jinsi alivyopoteza moja ya nafasi kubwa katika taaluma yake ya muziki kwa sababu ya ukosefu wa nauli.
Katika mahojiano ya hivi majuzi, Victoria alisimulia kuwa aliwahi kukutana na rapa na mjasiriamali maarufu wa Marekani, Sean Combs, maarufu kama P Diddy, wakati walipokuwa kwenye studio moja. Tukio hilo lilimfungulia mlango wa pili wa fursa kubwa, kwani alialikwa tena kwa ajili ya kufanya kazi kama vocal producer kwenye wimbo wa mwanamuziki Cassie, aliyekuwa mchumba wa Diddy kwa muda mrefu.
Hata hivyo, licha ya msisimko wa mwaliko huo, Victoria alisema hakuweza kuhudhuria kipindi cha pili cha kurekodi kwa sababu hakumudu gharama ya nauli ya teksi wala treni kwenda studio.
“Niliitwa tena ili kusaidia kurekodi sauti kwa ajili ya Cassie, lakini wakati huo sikuwa na hata senti ya nauli. Sikuwa na teksi, wala hata nauli ya treni,” alieleza kwa masikitiko.
Kauli hiyo imewagusa mashabiki wengi mitandaoni, wengi wakimsifia kwa ujasiri wa kushiriki hadithi ya wakati mgumu maishani mwake, huku wengine wakihuzunishwa na namna talanta inaweza kukosa kung’aa kutokana na changamoto za kifedha.
Victoria Kimani amekuwa mmoja wa wasanii wa kike wa Kenya waliowahi kutambulika kimataifa, akifanya kazi na majina makubwa katika muziki wa Afrika na Marekani. Hadithi yake inasisitiza umuhimu wa msaada kwa wasanii chipukizi, hasa wanapokuwa katika hatua za mwanzo za taaluma zao.