
Wachezaji kumi na moja wapya wameitwa kwenye kikosi cha mwanzo cha Harambee Starlets ili kuanza maandalizi ya mechi zijazo za kufuzu kwa mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika kwa wanawake ambapo itamenyana na Tunisia katika mechi ya mikondo miwili kuanzia tarehe ishirini na moja mwezi huu.
Kocha mkuu wa Harambee Starlets Bin Odeba amejumuisha kwenye timu hiyo walinda lango Vivian Shionzo wa timu ya Kibera soccer girls na Venda Abongo wa timu ya Kisped Queens katika jitihada za kuboresha kikosi hicho.
Safu ya ulinzi ina Elizabeth Ochaka ambaye aliandikisha matokeo bora katika timu ya junior starlet na atajiunga na wachezaji wapya wakiwemo Bernadet Atieno wa Kised Queens Alice Mideri wa Vihega Queza na Tabitha Amoita wa ulinzi Starlets.
Wachezaji wengine waliotajwa ni Mary Nthambi wa Kenya polisi na Janet Momo wa Kibera soccer women pamoja na mwenzake Ivona Idagiza miongoni mwa wengine. Timu hiyo itaingia kambini Jumatatu juma lijalo kujiandaa kwa mechi hizo zitakazochezwa tarehe ishirini na moja mwezi huu jijini Nairobi na kisha timu hiyo itasafiri kuelekea Tunisia kwa mechi ya marudiano tarehe ishirini na tano mwezi huu.