Tasnia ya muziki wa rap nchini Kenya imewaka moto baada ya Wakuu Music kutoa onyo kali kwa wasanii Toxic Lyrikali na Breeder LW, kufuatia kuibuka kwa diss tracks nne zilizowalenga wasanii wengine kama Trio Mio na Maandy.
Akiongea kwa hisia, Wakuu Music alimkosoa Toxic Lyrikali, akibainisha tofauti kubwa iliyopo kati yao. Alisisitiza kuwa yeye ni msanii aliyewekeza kikamilifu kwenye kazi yake na kutengeneza jina lake kupitia muziki, huku akimtaja Toxic kama mtu anayejenga jina lake zaidi kupitia mitandao ya kijamii.
Akimgeukia Breeder LW, Wakuu Music alimtuhumu kuwa msanii anayezungumza kupita kiasi na kutafuta “kiki” kupitia mivutano ya mtandaoni. Alipuuzilia mbali madai kuwa Breeder na kundi lake wanapanga njama ya kumshambulia, akieleza kuwa hayo ni mbinu za kutafuta umaarufu wa haraka usio na msingi.
Kwa upande wa Trio Mio, Wakuu Music amemtaja kama kijana ambaye hawafikia kwenye kiwango cha kumkabili, akieleza kuwa mawasiliano yao ya awali hayakuzaa matokeo yoyote na kwamba Trio hapaswi kuvutwa kwenye drama anazodai kusukwa na Breeder.
Maandy pia aliingia kwenye orodha ya walioshambuliwa, ambapo Wakuu Music alidai kuwa msanii huyo alijaribu kutumia mahusiano ya kimapenzi na Breeder LW kama njia ya kupata umaarufu. Alisisitiza kwamba mvutano huu haupaswi kuwa tiketi ya Maandy kujipandisha kimuziki.
Wakuu Music pia aligusia kwamba masuala yoyote yanayomhusu Octopizzo yanaweza kushughulikiwa kiutulivu bila drama za mitandaoni. Hata hivyo, alituma onyo kali kwa yeyote anayefikiria kumjibu, akisema kuwa akipata majibu kutoka kwao ataweka wazi tabia zao mtandaoni na hivyo kusisitiza wasijaribu kujibizana naye.
Sakata hilo limezidi kuchochea mjadala mitandaoni, huku mashabiki wakisubiri kuona iwapo wasanii waliolengwa watatoa majibu yao au kama mvutano huu wa rap utaendelea kupamba moto.