
Wanamuziki wa Injili kutoka nchini Uganda wamefunguka Kwanini Tamasha la msanii mwenzao Levixone halikupata mapokezi mazuri huko Kololo Airstrip wikiendi iliyopita.
Kulingana na Justine Nabbosa, waimbaji wa nyimbo za injili hawapati upendo wa kutosha na uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya waumini wa kikristo.
“Matamasha yetu hayavutii umati mkubwa kwa sababu Wakristo hawatusaidii. Siku zote wanatuona tukitumbuiza kanisani bure, jambo ambalo linawazuia kuja kwenye matamasha yetu,” anasema Justine Nabbosa.
Msanii wa Injili Betty Namaganda anasema, “Wakristo wanafikiri tunapaswa kubaki kanisani tukiimba bure lakini sisi pia tunahitaji pesa za kujikimu kimaisha. Napenda kuvishukuru vyombo vya habari vya kidunia kwa kutusaidia kutangaza show zetu”.
Utakumbuka mwaka 2018, Levixone aliweka rekodi ya kuwa mwanamuziki wa kwanza wa nyimbo za injili kuuza tiketi zote (sold out) za show yake aliyoiita “Turn The Reply” katika ukumbi wa Lugogo Cricket Oval huko nchini Uganda kabla ya kuhamia Kololo Airstrip.