
Watangazaji maarufu wa Radio 47, Alex Mwakideu na Emmanuel Mwashumbe, wamemtolea uvivu msanii Bahati kufuatia kauli yake kwamba angeweza kununua kituo cha Radio 47 pamoja na TV47 na kisha kumpa mke wake, Diana Marua, nafasi ya ubosi ili amsimamie mtangazaji Fred Arocho.
Katika kipindi cha asubuhi cha kituo hicho leo, Mwakideu na Mwashumbe walionekana kukerwa na matamshi ya Bahati, wakimtaka aache kujisifu na kudanganya mashabiki wake kuhusu uwezo wake kifedha. Walisema kuwa madai ya Bahati ni ya uongo kwani hana uwezo wa kununua kampuni ya Cape Media, wamiliki wa Radio 47 na TV47.
Kauli ya Bahati ilikuja baada ya Arocho kumshinikiza kutimiza ahadi yake ya shilingi milioni moja aliyoitoa kwa Harambee Stars. Msanii huyo alijibu kwa kejeli akidai kwamba akikasirika anaweza hata kununua kituo hicho na kumfanya Diana Marua kuwa bosi wa Arocho.
Hata hivyo, watangazaji hao walisema maneno ya Bahati hayana msingi, wakimtupia vijembe kwamba kama kweli ana uwezo huo, basi aanze kwanza kwa kumudu mishahara yao. โWee huna pesa! Usiwadanganye watu,โ waliongeza kwa dhihaka, wakimshauri aendelee na kazi yake ya muziki badala ya kuingilia masuala ya vyombo vya habari.
Hali hii imezua gumzo mitandaoni, huku mashabiki wakigawanyika kati ya wanaomuunga mkono Bahati na wale wanaosema amejipata pabaya baada ya kuwakera watangazaji wenye ushawishi mkubwa.