Kampuni ya Meta kupitia huduma yake ya ujumbe maarufu, WhatsApp, imeanza kufanya majaribio ya mwonekano mpya kwa watumiaji wa simu za iPhone.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kampuni hiyo, toleo hilo jipya litaendana na design ya mfumo mpya wa iOS 26, ambao umepewa jina la Liquid Glass kutokana na muonekano wake wa kisasa, unaovutia na wenye ufanisi wa hali ya juu.
Katika mwonekano huo mpya, WhatsApp itakuwa na interface safi zaidi, yenye mipangilio ya kisasa na themes zilizoboreshwa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinganisha muundo wa programu hiyo na mabadiliko mapya ya mfumo wa iOS.
Mabadiliko haya yanatarajiwa kuanza kutolewa rasmi hivi karibuni kwa watumiaji wote wa iOS, ingawa baadhi ya watumiaji wa toleo la majaribio (beta testers) tayari wameanza kuyaona mabadiliko hayo.
Kwa sasa, WhatsApp bado haijatangaza tarehe rasmi ya uzinduzi wa mwonekano huu mpya, lakini inaelezwa kuwa utatolewa kwa awamu kwa watumiaji kote duniani katika kipindi kifupi kijacho.
Hii ni ishara nyingine kwamba WhatsApp inaendelea kuwekeza katika kuboresha uzoefu wa mtumiaji, hasa kwa wale wanaotumia vifaa vya Apple.