Msanii nyota wa muziki nchini Kenya, Willy Paul, ametangaza hadharani kuwa hatofanya kazi ya pamoja tena na msanii wa Sauti Sol, Bien-Aimé Baraza baada ya tukio la matusi studioni.
Akifafanua uamuzi wake, Willy Paul ameeleza kuwa wakati wa ushirikiano wao wa awali alikumbana na mazingira magumu yenye matusi na maneno ya kudhalilisha. Amedai kuwa wakati wa kurekodi wimbo wao wa pamoja, alikumbana na matusi ya mara kwa mara bila sababu za msingi wakiwa studioni, hali iliyomfanya ajihisi kudhalilishwa na kuumizwa kisaikolojia.
Miaka mitano iliyopita, wawili hao walitoa wimbo uitwao “Kamati ya Roho Chafu”, uliopata mafanikio makubwa sokoni. Hata hivyo, Willy Paul sasa amefichua kuwa nyuma ya mafanikio hayo kulikuwa na kumbukumbu chungu isiyofurahisha.
Kwa sasa, msanii huyo ameweka msimamo thabiti kuwa hataki kurudia makosa ya zamani, akisisitiza kuwa hakuna uwezekano wa ushirikiano mwingine kati yake na Bien katika siku zijazo.