
Msanii wa muziki nchini Kenya, Willy Paul, ameibua mjadala mtandaoni baada ya kujitokeza kama mshauri nasaha kwa wanaume, akiwataka kuweka kipaumbele maendeleo yao binafsi badala ya kutumia muda mwingi kuwafuata wanawake.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Willy Paul aliwahimiza wanaume kuelekeza nguvu na muda wao katika kutafuta fedha na kujijenga kimaisha. Alisisitiza kuwa tabia ya kuwabembeleza wanawake kupita kiasi inaweza kuwapotezea muda muhimu na kuwazuia kufanikisha malengo yao ya maisha.
Kauli hiyo imezua maoni mseto miongoni mwa mashabiki, hasa ikizingatiwa kuwa inakuja siku moja tu baada ya kumshauri msanii mwenzake, Okello Max, ajikite zaidi katika kazi yake ya muziki. Alionya kuwa mienendo hiyo inaweza kuhatarisha mustakabali wa taaluma yake.
Willy Paul, anayejulikana kwa mitazamo yake yenye utata, ameendelea kutumia mitandao ya kijamii kama jukwaa la kutoa ushauri na maoni kuhusu masuala ya kijamii na maisha ya vijana.