
Rapa anayekuja kwa kasi nchini Kenya, Toxic Lyrikali, ameandika historia baada ya wimbo wake “Chinje” kufikisha views milioni 10 kwenye mtandao wa YouTube ndani ya kipindi cha miezi tisa tangu uachiwe rasmi.
Takwimu hizi zimempa nafasi kubwa katika muziki wa Afrika Mashariki, zikimuweka kwenye ramani kama moja ya vipaji vipya vinavyoibuka kwa nguvu.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Toxic Lyrikali ametoa shukrani kwa mashabiki wake wote waliomuunga mkono, akisisitiza kuwa mafanikio hayo yasingewezekana bila upendo na uaminifu wao. Aidha, ameahidi kuendelea kuwapa mashabiki wake ngoma kali zaidi katika siku zijazo.
Wimbo “Chinje” umekuwa gumzo kwa mashabiki kutokana na midundo yake ya kipekee na ujumbe unaoendana na ladha ya muziki wa kizazi kipya. Wachambuzi wa muziki wanaona mafanikio haya kama kielelezo cha jinsi wasanii wapya wanavyoweza kufika mbali kwa kutumia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali.