Mwanamuziki na mtunzi wa nyimbo kutoka Kenya, Xenia Manasseh, ameandikisha historia baada ya kupokea uteuzi wake wa kwanza kabisa wa Grammy Awards kwa mchango wake katika albamu ya “Escape Room” ya Teyana Taylor, ambayo imeteuliwa katika kipengele cha Best R&B Album.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Xenia hakuweza kuficha furaha yake, akieleza kuwa ni uteuzi wake wa kwanza wa Grammy na akisisitiza kuwa siku hiyo ilikuwa maalum zaidi kwani ilikuwa pia siku ya kuachiwa kwa EP yake mpya “Maybe II”.
Mrembo huyo ameongeza kuwa anashukuru Mungu kwa hatua hiyo ila ameshangazwa namna yeye na mtayarishaji Kvn Hrtlss kutoka nchini Uganda wamepata mafanikio hayo, akieleza kuwa bado haamini kilichotokea.
Xenia Manasseh,, sasa anajiunga na Eddy Kenzo kutoka Uganda ambaye amechaguliwa kuwania kipengele cha Best African Music Performance kupitia wimbo wake “Hope & Love” aliomshirikisha mwanamuziki na mtayarishaji maarufu wa vyombo vya muziki, Mehran Martin.