
Msanii maarufu wa Hip Hop, Young Thug, ameibua gumzo baada ya kueleza dhamira ya kuachana na muziki na kuhamia kwenye ulimwengu wa ustreaming. Akiwa mubashara na streamers maarufu Adin Ross na Neon, alieleza kuwa amechoka na muziki na anatamani kujikita katika maisha ya utangazaji wa moja kwa moja.
Kauli hiyo imeibua mijadala mitandaoni, wengi wakihusisha hatua hiyo na kuvutiwa kwake na maisha ya streamers, ambayo alielezea kuwa ni huru, ya kusafiri mara kwa mara na yenye mapato makubwa kwa muda mfupi.
Pamoja na hayo, hakuna taarifa rasmi kutoka kwa menejimenti yake, na baadhi ya wachambuzi wanaamini huenda kauli hiyo ni sehemu ya mbinu za kutangaza albamu yake mpya “UY Scuti”, inayotarajiwa kutoka mwezi huu wa Juni.
Young Thug, ambaye amekuwa mmoja wa vinara wa muziki wa trap kwa zaidi ya muongo mmoja, bado anapewa nafasi na mashabiki kuendelea na kazi yake ya muziki licha ya dalili hizo za kutaka kubadili mwelekeo.