
Kampuni ya YouTube imeanza kutekeleza mabadiliko mapya kwenye video player wake kwa lengo la kuimarisha uzoefu wa mtumiaji. Katika mwonekano huu mpya, YouTube imeleta maboresho ya kimuonekano kwa kubadilisha sura ya baadhi ya vitufe kuwa na miundo ya kisasa kama duara (circular) na pill-shaped.
Mabadiliko haya yanahusisha vitufe muhimu kama vile Play/Pause, Next, na sehemu za video zinazoonesha chapters ambazo sasa zitakuwa na pembe za duara, tofauti na muundo wa zamani uliokuwa na pembe nne. Aidha, kitufe cha sauti (volume) kimehamishwa kutoka sehemu yake ya awali na sasa kitaonekana upande wa kulia wa video player.
Lengo kuu la mabadiliko haya ni kufanya matumizi ya YouTube yawe rahisi zaidi, ya kisasa, na ya kuvutia kwa macho, hasa kwa watumiaji wa simu janja na vidhibiti vya kugusa (touch controls). Hii pia ni sehemu ya juhudi za YouTube kuendana na mitindo mipya ya kiteknolojia na kuboresha muingiliano wa watumiaji na majukwaa yao.
Mabadiliko haya yanatarajiwa kusambazwa kwa watumiaji wote duniani kwa awamu, hivyo watumiaji wanaweza kuanza kuyaona mabadiliko haya hivi karibuni ikiwa bado hawajayapokea.