Mfanyibiashara na sosholaiti maarufu, Zari Hassan, alijikuta akibubujikwa na machozi baada ya mumewe, Shakib Cham, kupigwa knockout vibaya na msanii Rickman Manrick katika pambano la masupastaa lililoshuhudiwa usiku wa Jumamosi, 30 Agosti 2025, ndani ya MTN Arena, Lugogo.
Pambano hilo lililokuwa limevuta maelfu ya mashabiki lilimalizika mapema katika raundi ya pili, baada ya Rickman kumshushia Shakib ngumi nzito pande zote za kichwa na kumwangusha chini akipoteza fahamu. Umati ulilipuka kwa shangwe, lakini macho yote yalihamia moja kwa moja kwa Zari, aliyekuwa safu ya mbele, akishuhudia mume wake akizimwa ringini.
Awali, Zari alionekana akishangilia kwa nguvu akimhimizia mumewe kupambana, lakini alibadilika ghafla na kuangua kilio mara tu Shakib alipoanguka chini bila msaada. Alimkimbilia ulingoni, akimshika na kumfariji huku akibubujikwa na machozi, jambo lililoacha taswira ya aibu mbele ya umati na kamera zilizokuwa zikirekodi kila tukio.
Mitandaoni, mashabiki hawakuchelewa kumrushia vijembe, wakimuita “First Lady wa Knockout”, huku wengine wakisema “hata machozi ya Zari hayawezi kufuta aibu ya kipigo cha Shakib.” Wengine walimkejeli kuwa safari hii si biashara zake wala mitindo yake ya kifahari iliyokuwa gumzo, bali machozi yake ringini.
Rickman kwa upande wake aliendeleza rekodi yake ya ushindi, akipata ushindi wa pili katika michezo ya masupastaa baada ya kumbwaga pia msanii Grenade Official mnamo Desemba 2024. Kwa Shakib na Zari, pambano hili limeacha kumbukumbu chungu, knockout kwa ulingo, na machozi kwa jukwaa la mbele.