
Msanii maarufu wa Dancehall nchini Uganda, Ziza Bafana, ameibuka na lawama kali dhidi ya waandaaji wa matamasha (promoters) na viongozi wa serikali, akiwalaumu kwa kuchelewesha maendeleo ya muziki wa Uganda na kuzuia wasanii wa taifa hilo kuvuka mipaka kimuziki.
Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini humo, Bafana alisema kuwa promoters wengi nchini Uganda wamekuwa wakipendelea kufanya kazi na wasanii wasio na mpangilio wala chapa rasmi ya kisanaa. Kwa mujibu wa Bafana, hali hiyo imekuwa ikizuia maendeleo ya wasanii waliowekeza kikamilifu katika ubunifu, utaratibu na ujenzi wa chapa zao.
“Waandaaji wa matamasha hawawaheshimu wasanii. Wanataka tu kufanya kazi na wale wasio na mpangilio wowote. Wakiona msanii aliye na chapa nzuri na amejiweka vyema, wanampiga vita hadi aanguke,β alisema kwa hisia.
Kauli hiyo imeungwa mkono na mashabiki na wadau wa tasnia ya muziki ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia mazingira magumu ambayo wasanii wa Uganda hukabiliana nayo licha ya uwekezaji mkubwa katika utayarishaji na utangazaji wa kazi zao.
Aidha, Ziza Bafana hakuishia kwa promoters pekee. Alielekeza lawama pia kwa viongozi wa serikali ya Uganda kwa kile alichokitaja kama ukosefu wa heshima na kuthamini sanaa.
Β βViongozi wetu hawaheshimu sanaa. Hawaoni uzuri wake. Itahitaji mabadiliko makubwa ili sanaa iheshimiwe, na hapo ndipo tutaanza kuona maendeleo,β aliongeza.
Kauli ya Ziza Bafana inakuja wakati ambapo mjadala kuhusu hadhi ya wasanii na mchango wa sekta ya burudani katika uchumi na utambulisho wa taifa unazidi kushika kasi, huku wasanii wengi wakihamasisha mageuzi katika mfumo wa usimamizi wa sanaa nchini Uganda.
Mashabiki wamekuwa wakisubiri kuona kama kauli za Bafana zitachochea mjadala mpana zaidi unaoweza kuleta mabadiliko chanya kwa tasnia ya muziki nchini humo.