Entertainment

Megan Thee Stallion Aonyesha Hasira kwa Mashabiki wa Tory Lanez Walio na Mashaka Kuhusu Kesi ya Risasi

Megan Thee Stallion Aonyesha Hasira kwa Mashabiki wa Tory Lanez Walio na Mashaka Kuhusu Kesi ya Risasi

Rapa maarufu kutoka Marekani, Megan Thee Stallion, ameamua kupambana hadharani na mashabiki wa Tory Lanez ambao bado wanakanusha ukweli kwamba mwanamuziki huyo alimpiga risasi licha ya uamuzi wa mahakama ya juri mjini Los Angeles kuthibitisha hilo.

Kupitia ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Megan ameonesha kuchoshwa na mashambulizi ya mfululizo kutoka kwa baadhi ya watu wanaoendeleza kampeni ya kumdhalilisha, huku akimtaja Tory Lanez kama shetani anayeendelea kumletea mateso hata baada ya hukumu.

“Muda umefika muache kunitesa. Mlikuwa na nafasi ya kusema mliyotaka mahakamani. Mnaendelea tu na uongo  ni kama mapepo,” Megan alisema kwa hasira.

Megan ambaye anaendelea na kazi yake ya muziki, ameweka wazi kuwa bado anapitia changamoto za kiakili kutokana na matukio hayo, hasa kutokana na mashambulizi ya mfululizo kutoka kwa baadhi ya watu mitandaoni. Ameongeza kuwa bado anaumizwa na namna watu wanavyopuuza ukweli na kumshambulia yeye badala ya kumwajibisha Tory.

“Mahakama ilizungumza. Ukweli ulidhihirika. Lakini bado naandamwa kana kwamba mimi ndiye mwenye makosa.” aliongeza.

Kauli hiyo imeibua mjadala mkali mtandaoni huku mashabiki wake wakimtetea vikali na kuitaka jamii kumheshimu kama manusura wa tukio la vurugu. Wengine, hususan wafuasi wa Tory, bado wanaonekana kushikilia imani tofauti, jambo linalozua sintofahamu kubwa.

Tory Lanez tayari anatumikia kifungo gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumpiga Megan risasi mwaka 2020, tukio lililotokea baada ya sherehe usiku.

Huu ni mwendelezo wa mvutano kati ya Megan na Tory ambao umegusa si tu mashabiki wao, bali pia wasanii na wanaharakati wa haki za wanawake kwenye tasnia ya muziki duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *