
Mwanamuziki na mtunzi mashuhuri Victoria Kimani amezua gumzo mitandaoni baada ya kudokeza kuhusu gari la kifahari aina ya Rolls Royce linalodaiwa kuwa la bandia, ambalo linapigiwa debe katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwenye mahojiano yake hivi karibuni, Victoria alirusha dongo la chinichini kwa mtu mashuhuri ambaye hakumtaja moja kwa moja, akidai kuwa anajigamba na gari la kifahari lisilo halisi.
“Si kila Rolls Royce ya buluu unayoiona mitaani ni halisi. Wengine wanapenda kuishi kwa kiki kuliko uhalisia,” alisema Kimani.
Ingawa hakumtaja jina mhusika, mashabiki na wachambuzi wa mitandao walihisi kuwa ujumbe huo umeelekezwa kwa kwa staa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz ambaye hivi karibuni ameonekana mara kwa mara akipiga picha na gari la kifahari la rangi ya buluu katika hafla mbalimbali.
Kauli ya Kimani imezua maoni mseto, baadhi wakimpongeza kwa kusema ukweli huku wengine wakimshutumu kwa kuanzisha mzozo usio na msingi. Wafuasi wa Diamond wamemkingia kifua msanii wao, wakisisitiza kuwa gari hilo ni halisi na lilinunuliwa kihalali.
Diamond Platnumz bado hajajibu hadharani kuhusu suala hilo, lakini mijadala inaendelea kushika kasi mitandaoni huku mashabiki wakingoja kuona iwapo atatoa majibu au kulipuuza kabisa.