Mashindano ya Soka ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) yanaingia katika hatua ya nusu fainali kesho, huku macho ya mashabiki wa soka barani Afrika yakielekezwa nchini Uganda na Tanzania ambako mechi hizo zitachezwa.
Katika mchezo wa kwanza, mabingwa wa zamani Morocco watavaana na Senegal katika Uwanja wa Mandela uliopo mjini Kampala, Uganda. Morocco wanatafuta kurejesha hadhi yao ya ubabe barani, lakini wanakutana na Senegal iliyoonyesha ubora kwa kuing’oa Uganda kwa ushindi wa bao 1-0 kwenye robo fainali.
Kwa upande mwingine, Madagascar watamenyana na Sudan katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Tanzania. Madagascar waliingia nusu fainali kwa kishindo baada ya kuilaza Harambee Stars ya Kenya 4-3 kupitia mikwaju ya penalti, kufuatia sare ya bao 1-1. Sudan wao walifuzu kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Algeria.
Mechi hizi zinatarajiwa kuwa na ushindani mkali na kusisimua, huku kila timu ikisaka nafasi ya kuingia fainali na kuweka historia kwenye CHAN ya mwaka huu.