Msanii wa muziki kutoka Kenya, Willy Paul, ametoa wito kwa umma kumsaidia kuwatambua wahalifu waliovamia na kupora duka lake la pombe. Tukio hilo lilinaswa kwenye kamera za CCTV ambazo sasa msanii huyo ameziweka wazi hadharani kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Willy Paul amesema kuwa tayari amepata video kamili ya tukio hilo, ikionyesha wazi sura za wahusika waliohusika. Kwenye video hiyo, anaeleza kuwa mtu mmoja aliyekuwa amevaa koti jeupe na mwanamke aliyeonekana akiwa amevalia mavazi meusi yote ndio wanaoonekana kuongoza uvamizi huo.
Msanii huyo amehimiza umma kutoa taarifa yoyote itakayosaidia katika kuwatambua wahusika hao, akisisitiza kuwa polisi wameanza uchunguzi na wamechukua hatua za haraka kuhakikisha waliohusika wanakamatwa.
Tukio hilo limezua hisia kali mitandaoni baada ya CCTV kuonyesha namna uvamizi huo ulivyotekelezwa, ambapo kundi la watu liliingia kwa nguvu na kupora bidhaa mbalimbali kwenye duka hilo la pombe, lililodaiwa kushambuliwa na wahuni waliopangwa.