Staa wa muziki Willy Paul ametangaza kurejea kwa huduma katika duka lake la vileo, Pozze Liquor, siku chache baada ya wahuni kuvamia na kuharibu mali ya thamani ya mamilioni ya fedha.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Willy Paul ameeleza kuwa duka hilo limekarabatiwa kikamilifu, limejazwa upya bidhaa, na sasa limeboreshwa mara kumi zaidi.
Hitmaker huyo wa Ngunga, ameshukuru mashabiki wake kwa maombi na usaidizi waliompa wakati wa kipindi kigumu, akisisitiza kuwa uharibifu uliotokea haukuwa mkubwa kuliko imani yake kwa Mungu.
Duka la Pozze Liquor lililoko jijini Nairobi linajulikana kwa kuuza vileo vya kiwango cha juu na limekuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa msanii huyo. Mashabiki wengi wamempongeza kwa kurejea kwa nguvu upya, wakimtaja kama mfano wa uvumilivu na bidii katika biashara.