Mwigizaji maarufu wa Kenya, Nyce Wanjeri, amethibitisha kuwa baadhi ya mali zake zimepigwa mnada kufuatia changamoto kubwa za kifedha anazopitia kwa sasa.
Kupitia mitandao yake ya kijamii, amesema kuwa ameshindwa kulipa madeni yake kwa wakati, hali iliyosababisha madalali (auctioneers) kuanza kuuza mali zake ili kufidia fedha wanazodaiwa.
Mwigizaji huyo amesema hali hiyo imemweka kwenye wakati mgumu zaidi, kwani mbali na kupoteza mali, familia yake pia inakabiliwa na tishio la kufurushwa wanakoishi baada ya kushindwa kulipa kodi kwa miezi kadhaa.
Ameeleza pia kuwa binti yake ameshindwa kuendelea na masomo kutokana na kushindwa kulipiwa ada ya shule, jambo linaloongeza uzito wa matatizo anayokabiliana nayo kwa sasa.
Hata hivyo,Wanjeri, anayejulikana kwa umahiri wake katika tamthilia ya Auntie Boss, amewataka mashabiki wake waendelee kumwombea na kumuunga mkono katika kipindi hiki kigumu.