Mfumo wa kompyuta wa Windows 10 umefikia tamati rasmi, ambapo jana, Oktoba 14, 2025, ilikuwa siku ya mwisho kwa Microsoft kutoa msaada wa kiufundi na masasisho ya kiusalama kwa mfumo huo maarufu.
Windows 10 ilizinduliwa rasmi mnamo Julai 29, 2015, na kwa kipindi cha miaka 10, imekuwa moja ya mifumo inayotumika zaidi duniani, hasa katika sekta za elimu, biashara na matumizi ya kawaida ya nyumbani.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Microsoft, watumiaji wa mfumo huo wanahimizwa kuhamia Windows 11, ambao ni mfumo wa kisasa zaidi wenye usalama wa hali ya juu, kasi ya utendaji na maboresho ya kiutumiaji.
Ingawa Microsoft haijawazuia watumiaji kuendelea kutumia Windows 10, kampuni hiyo imesisitiza kuwa kuendelea kutumia mfumo huo baada ya ukomo wa msaada kunahatarisha usalama wa kompyuta na data binafsi. Hii ni kwa sababu hakutakuwa na tena updates za kiusalama, jambo linaloweka wazi mianya kwa virusi na mashambulizi ya mitandaoni.
Kwa watumiaji wanaotumia kompyuta zilizounganishwa kwenye mtandao (internet), hali hii ni hatari zaidi kwani mashambulizi ya kimtandao yanaweza kuathiri vifaa vyao na kusababisha upotevu wa taarifa muhimu.
Hatua Za Kuchukua
- Angalia kama kompyuta yako ina uwezo wa kuendesha Windows 11
- Fanya backup ya data zako kabla ya kuhamia mfumo mpya
- Wasiliana na mtaalamu wa IT kwa msaada wa kuboresha mfumo
Kwa sasa, Windows 11 ndiyo njia salama na sahihi kwa watumiaji wanaotaka kuendelea kufurahia huduma bora na salama kutoka Microsoft.