Mchekeshaji na mwanaharakati Eric Omondi ametetea vijana wa Gen Z kufuatia madai kwamba hawakujitokeza kushiriki uchaguzi mdogo uliofanyika Novemba 27, ambapo idadi ya wapiga kura ilikuwa ndogo kushinda matarajio.
Kupitia mitandao ya kijamii, Omondi amesema kutoshiriki kwao hakukuwa dalili ya kutojua umuhimu wa uchaguzi, bali ni hatua ya kujiondoa kwenye michakato ambayo haina manufaa kwao. Amefafanua kuwa uchaguzi huo haukuwa juu ya mustakabali wa vijana, bali ni mapambano kati ya wanasiasa na makundi yenye maslahi yao binafsi, hali aliyoiita vita vya kisiasa.
Kwa mujibu wake, vijana walibaki pembeni kwa sababu hawangefaidika lolote kutokana na uchaguzi huo, na hivyo hawakuona sababu ya kushiriki. Amepinga vikali juhudi za kuwalaumu Gen Z kwa idadi ndogo ya waliojitokeza kupiga kura, akisema ni makosa kuwatupia lawama wakati hawahusishwi kikamilifu katika maamuzi yanayowahusu.