Mchekeshaji na mtangazaji wa Kenya, Oga Obinna, ameibuka kumtetea kwa nguvu mwandishi wa habari wa CNN, Larry Madowo, kufuatia kauli ya mpambe wa Rais Samia Suluhu Hassan aliyepinga na kupuzilia mbali ripoti ya chombo hicho kuhusu machafuko ya uchaguzi nchini Tanzania.
Akiwa hewani kupitia Obinna TV, Obinna ameonekana kukerwa na hatua ya mpambe huyo kuhoji uhalali wa taaluma ya Madowo. Amesisitiza kuwa Madowo ni mwandishi mwenye tajriba ya muda mrefu katika vyombo vikubwa vya habari duniani na hawezi kuripoti taarifa za uongo kama inavyodaiwa.
Obinna ameongeza kuwa ni muhimu viongozi na wasaidizi wao kuheshimu kazi ya wanahabari, hasa wale wanaofanya kazi katika vyombo vya kimataifa, kwani wanahabari hao hufuata misingi ya uandishi wa kitaaluma na huchunguza kwa kina kabla ya kuripoti.