Msanii wa Bongo Fleva, Harmonize, ameibua taharuki mitandaoni baada ya kutangaza wazi kuwa yuko tayari kuzichapa na Baba Levo kufuatia kauli zinazomkera kutoka kwa mbunge huyo ambaye pia ni msanii na mtangazaji.
Hii inakuja baada ya Baba Levo kudai kuwa Diamond Platnumz ndiye aliyemtoa Harmonize mavumbini, kauli ambayo Harmonize ameipinga vikali na kuiita ya kumdhalilisha. Ameeleza kuwa safari yake ya muziki imejengwa kwa damu, jasho, na juhudi binafsi si msaada wa mtu yeyote.
Harmonize amesema amechoshwa na maneno ya Baba Levo na sasa yuko tayari kumkabili ana kwa ana ikiwa ndio lugha pekee atakayoielewa. Ameongeza kuwa ukimya wake umechukuliwa vibaya, na hivyo anataka kuweka mipaka na kulinda heshima yake.
Harmonize ametoa msimamo mkali akiwataka wanaoandika habari kumhusu kuanza kwa kumtaja Mungu pekee, na si kumhusisha na mtu yeyote katika kutengeneza mafanikio yake.
Kwa mujibu wa msanii huyo, kumhusisha na Diamond ni kutaka kumpotosha hadharani kuhusu safari ambayo ameijenga mwenyewe tangu akiwa chini kabisa kwenye muziki.