Mtandao wa kijamii wa TikTok umeanzisha rasmi programu (app) mpya inayoitwa PineDrama, inayolenga kutoa burudani ya micro-dramas yaani video fupi za mfululizo pamoja na filamu zenye simulizi fupi lakini zenye mvuto mkubwa kwa watazamaji.
Kwa mujibu wa TikTok, PineDrama imeundwa mahsusi kwa ajili ya watumiaji wanaopenda hadithi fupi zilizojaa ubunifu, ambapo maudhui yote yatakuwa katika mfumo wa episodes na series, yakitoa uzoefu unaofanana na tamthilia au filamu fupi zinazofuatana.
Tofauti na majukwaa mengi ya kidijitali, TikTok imesisitiza kuwa PineDrama haitakuwa na matangazo kabisa, na itapatikana bure kwa watumiaji wake, jambo linalolenga kuwapa watazamaji uhuru wa kufurahia maudhui bila usumbufu.
Kwa sasa, programu hiyo imeanza kupatikana katika baadhi ya nchi, huku TikTok ikieleza kuwa itazinduliwa rasmi kwa watumiaji wote duniani katika kipindi kijacho. Hatua hii inaonyesha dhamira ya TikTok kupanua wigo wa burudani ya kidijitali na kuwapa nafasi wabunifu wa maudhui kusimulia hadithi kwa mbinu mpya na za kisasa.
Uzinduzi wa PineDrama unatarajiwa kuongeza ushindani katika sekta ya streaming na kufungua fursa mpya kwa waigizaji, waandishi na watayarishaji wa maudhui duniani.