Kampuni ya Microsoft inajiandaa kutikisa ulimwengu wa teknolojia mwaka huu kwa kuachia mfumo wake mpya wa uendeshaji, Windows 12. Windows 12 unatarajiwa kuwa mfumo mpya wa uendeshaji wa kompyuta wenye mabadiliko makubwa, hasa katika matumizi ya teknolojia ya akili bandia maarufu kama AI.
Kipengele kikubwa zaidi kitakuwa kuingizwa kwa AI moja kwa moja ndani ya mfumo wa Windows. AI ya Copilot itaunganishwa ndani ya mfumo wenyewe, badala ya kuwa programu ya kujitegemea kama ilivyokuwa hapo awali. Hii itasaidia watumiaji kupata msaada wa haraka katika kazi mbalimbali kama kuandika, kupanga kazi, kutafuta taarifa na hata kudhibiti baadhi ya mipangilio ya kompyuta.
Katika hatua nyingine mpya, baadhi ya huduma za AI ndani ya Windows 12 zitakuwa za kulipia kwa mfumo wa usajili (subscription). Hii ina maana kuwa watumiaji watakaotaka kutumia huduma za hali ya juu zaidi za AI watahitaji kulipia huduma hizo kila mwezi au kila mwaka.
Aidha, Windows 12 haitafanya kazi katika kila kompyuta. Mfumo huu utahitaji kompyuta zenye chip maalum yenye uwezo wa NPU- Neural Processing Unit, ambayo hutumika kushughulikia kazi za AI kwa ufanisi zaidi. Hivyo, baadhi ya kompyuta zenye processor za kawaida kama Intel Core i3 au i5 huenda zisipate mfumo huu mpya.
Kwa upande wa muonekano, Windows 12 itakuja na mwonekano mpya wa kisasa zaidi. Taskbar yake inatarajiwa kuwa ya aina ya floating yenye muonekano wa glass, unaofanana na muundo unaotumika katika mfumo wa macOS kwenye kompyuta za Mac za kampuni ya Apple.
Kwa ujumla, Windows 12 inatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika dunia ya kompyuta, hasa kwa kuifanya teknolojia ya AI kuwa sehemu ya matumizi ya kila siku ya watumiaji wa kompyuta.