Mwimbaji wa nyimbo za injili kutoka Tanzania Rose Muhando amekanusha madai kuwa hupikiwa chakula na watu wengine kutokana na ratiba yake yenye shughuli nyingi za muziki.
Muhando amesema kuwa licha ya kuwa na majukumu mengi katika kazi yake ya muziki, bado hupata muda wa kujiandalia chakula chake mwenyewe kwani ana uzoefu mkubwa wa mapishi.
Msanii huyo ameeleza kuwa ujuzi wake wa kupika ulianza tangu akiwa mdogo alipokuwa akiishi na shangazi yake katika mji wa Tanga, ambaye alimfundisha jinsi ya kuandaa vyakula mbalimbali vya nyumbani.
Kwa mujibu wa Muhando, mafunzo aliyoyapata kutoka kwa shangazi yake ndiyo yaliyomfanya awe na uwezo wa kupika hadi sasa, hivyo hana tatizo la kujipikia hata akiwa na ratiba kali ya kazi.
Kauli yake imekuja baada ya kupakia video kwenye mitandao ya kijamii akionyesha ustadi wake jikoni alipokuwa akiandaa chakula. Katika video hiyo, Rose aliwaomba mashabiki wake wamtathmini na kumpa alama kuhusu uwezo wake wa mapishi.