Kampuni ya Apple imezindua rasmi laptop mpya inayojulikana kama MacBook Neo, ambayo sasa imekuwa MacBook yenye bei ya chini zaidi katika familia ya MacBook. Hatua hii inaonyesha juhudi za Apple kufikia watumiaji wengi zaidi, hasa wale wanaotafuta laptop ya Apple kwa gharama nafuu.
MacBook Neo inakuja na chip ya A18 Pro, chip hii ndiyo ile ile inayotumika kwenye simu ya iPhone 16. Kwa lugha rahisi, ni kama “ubongo wa iPhone” sasa unatumika kwenye kompyuta ya laptop. Hii inaonyesha jinsi Apple inavyoendelea kuunganisha teknolojia zake kati ya simu na kompyuta.
Kwa upande wa matumizi, MacBook Neo imelenga zaidi watu wanaofanya kazi zisizohitaji nguvu kubwa ya kompyuta. Laptop hii inafaa sana kwa wanafunzi, wafanyakazi wa ofisini, na watu wanaotumia sana programu za kuandika nyaraka kama Microsoft Word pamoja na kazi nyingine rahisi za kila siku kama kuvinjari mtandaoni, kusoma, na kuandaa documents.
Licha ya kuitwa MacBook ya bei nafuu zaidi, bei yake bado inaweza kuonekana kubwa kwa baadhi ya watumiaji. MacBook Neo inauzwa kwa dola $599, ambazo ni takribani Shilingi za Kenya 77,000 hadi 80,000, kulingana na kiwango cha ubadilishaji wa fedha.
Uzinduzi wa MacBook Neo unaashiria mkakati mpya wa Apple wa kujaribu kuvutia watumiaji wa soko la chini na la kati, hasa wanafunzi na watu wanaotaka kuingia kwenye mfumo wa Apple bila kutumia fedha nyingi kama ilivyo kwa MacBook nyingine.