Msanii nyota wa muziki kutoka Uganda, Eddy Kenzo, amefichua sababu inayomfanya asiweze kufunga katika mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka huu.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Kenzo amesema kuwa anakabiliwa na changamoto kubwa ya kiafya ya vidonda vya tumbo (ulcers), hali ambayo humfanya ashindwe kukaa bila kula kwa muda mrefu. Msanii huyo ambaye pia ni mmiliki wa lebo ya Big Talent Entertainment amesema kufunga kwa saa nyingi kunaweza kuzidisha hali yake ya afya.
Kenzo ameeleza kuwa kutokana na matatizo hayo ya kiafya, amelazimika kusitisha kwa muda ibada ya kufunga ili kulinda afya yake.
Hata hivyo, licha ya kutofunga, Kenzo amesema bado anaunga mkono waumini wanaotekeleza ibada ya Ramadhani kwa kuwasaidia kwa chakula ili waweze kufuturu wakati wa jioni.
Kenzo anaungana na baadhi ya wasanii wengine wa Uganda kama Bebe Cool na Lil Pazo, ambao pia wanajulikana kuwa Waislamu lakini wamewahi kukiri hadharani kuwa hawafungi katika baadhi ya vipindi vya mwezi wa Ramadhani kutokana na sababu mbalimbali.