Mshambuliaji wa kimataifa wa Ujerumani, Kai Havertz, amekuwa shujaa wa Arsenal baada ya kufunga bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 89 dhidi ya klabu yake ya zamani, Bayer Leverkusen.
Katika mchezo huo wa hatua ya 16 bora uliopigwa kwenye dimba la BayArena, Arsenal walionekana kulemewa baada ya nahodha wa Leverkusen, Robert Andrich, kupachika bao la kuongoza mapema kipindi cha pili. Licha ya mashambulizi makali ya wenyeji, vijana wa Mikel Arteta walipambana na kuambulia sare ya 1-1, matokeo yanayowapa nafasi nzuri kuelekea mchezo wa marudiano jijini London.
Katika pambano lingine la kukata na shoka, mabingwa wa kihistoria Real Madrid wameendeleza ubabe wao kwa kuifunga Manchester City mabao 3-0 katika dimba la Santiago Bernabéu. Kiungo Federico Valverde aliziba vinywa vya mashabiki wa City kwa kufunga hat-trick safi ndani ya dakika 22 za kipindi cha kwanza. Licha ya jitihada za Erling Haaland na Kevin De Bruyne, safu ya ulinzi ya Madrid ilisimama kidete na kuizuia City kupata hata bao la kufutia machozi.
Kule Ufaransa, Paris Saint-Germain (PSG) wameonesha kwa nini wanatajwa kuwa miongoni mwa timu tishio msimu huu baada ya kuichapa Chelsea mabao 5-2. Chelsea walijitahidi kurudi mchezoni kupitia mabao ya Malo Gusto na Enzo Fernández, lakini ufundi wa Khvicha Kvaratskhelia aliyefunga mabao mawili ya mwishoni uliwahakikishia PSG ushindi mnono nyumbani.
Klabu ya Bodø/Glimt kutoka Norway aliicharaza Sporting CP mabao 3-0. Ushindi huo mnono nyumbani unaiweka timu hiyo katika nafasi ya kipekee ya kutinga hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya mashindano hayo makubwa duniani.