
Rapa maarufu 50 Cent amejitokeza waziwazi kupinga kauli ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu uwezekano wa kumsamehe Sean “Diddy” Combs, ambaye anakabiliwa na mashtaka mazito ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono na uhalifu wa kupanga.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, 50 Cent alionyesha kutoridhishwa na kauli ya Trump, akieleza kuwa Diddy amekuwa akiongea vibaya kuhusu Trump kwa muda mrefu, na hivyo si sahihi kwa kiongozi huyo wa zamani kufikiria kumsamehe mtu ambaye hakumuunga mkono.
“Alisema mambo mabaya sana kuhusu Trump, sio sawa. Nitawasiliana naye ili ajue jinsi ninavyohisi kuhusu mtu huyu.” aliandika Instagram
Kauli hii ya 50 Cent inakuja baada ya Trump kusema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba hajapokea ombi rasmi la msamaha kwa Diddy, lakini yuko tayari kuangalia ukweli wa kesi hiyo kabla ya kufanya uamuzi wowote.
Diddy anakabiliwa na mashtaka mazito ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono, njama ya uhalifu, na usafirishaji kwa ajili ya ukahaba. Iwapo atapatikana na hatia, anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani.
Uhusiano kati ya 50 Cent na Diddy umekuwa na mvutano kwa muda mrefu, na 50 Cent amekuwa akitoa maoni ya ukosoaji dhidi ya Diddy mara kwa mara. Kauli yake ya sasa inaonyesha nia ya kuzuia msamaha wowote kutoka kwa Trump kwa Diddy.